Hali Ya Ushirika Nchini

Vyama vya Ushirika vimekuwa sehemu muhimu ya maendeleo kwa miaka karibu 75 iliyopita. Hivyo ingawa vimepata matatizo na changamoto nyingi, ni wazi na imedhihirika kwamba hakuna chombo kingine zaidi ya Ushirika kinachoweza kuwaunganisha wakulima kuwa na sauti moja katika kuendesha shughuli zao za kiuchumi na ustawi wa jamii kwa ujumla. Ushirika pia hurahisisha Serikali kupitisha mipango yake ya maendeleo iweze kuwafikia wananchi kwa urahisi na uhakika mkubwa.

Aidha, baada ya Serikali kuvipa nafasi Vyama kushindana na sekta binafsi ilishuhudiwa Vyama vingi kuingia kwenye mkwamo kiuchumi na vingine kujikuta kwenye madeni makubwa ikiwa ni pamoja na SHIRECU (1984) LTD. Hata hivyo Serikali baada ya kuyaona hayo ilibadili mwelekeo na kuvitaka Vyama Vikuu kuwa wasimamizi na watoa huduma pekee kwa Vyama vya Msingi ili kupanua wigo wa mkulima kupata huduma stahiki, kwa sasa chama kikuu kinafanya yafuatayo:-

  1. Kufukiza maghala kila inapofikia msimu.
  2. Kutengeneza mizani na kuigawa kwa Vyama vya Msingi.
  • Kutoa huduma ya vitabu.
  1. Kutoa huduma ya Elimu ya Uandishi wa vitabu.
  2. Kuhamasisha wakulima kujiuna na vyama vya ushirika vya msingi.
  3. Kusafirisha mbegu za mazao kama pamba, dengu na choroko kwa kutumia magari yake
  • Kununua Dengu na choroko

 

Aidha, kwa kutoa huduma hizo chama kikuu kimekuwa kikipata ushuru ambao nao umekuwa ukibadilika takribani kila mwaka kwa kutokana kupanda na kushuka na kufanya chama kushindwa kujiendesha na kuhimili hali ya sasa.

Maendeleo ya Sekta ya Ushirika yanategemea sana nia thabiti na yenye tija kwa mustakabali wa maendeleo ya chama kikuu, Vyama vya Msingi na Mkulima kwa ujumla. Tayari Serikali imekwishajipambanua kwa nia yake thabiti ya kuimarisha Ushirika. Mambo yaliyofanywa na Serikali ni kama vile kurudisha mali za Ushirika, kuondoa wizi na ulaghai kwa Mkulima, kuimarisha na hata kubadili mifumo mbalimbali kama stakabadhi ghalani. Lengo likiwa ni kuimarisha Ushirika na kuufanya usonge mbele.