Mrajis Msaidizi wa Vyama vya ushirika Mkoa wa Shinyanga, Kakozi Ibrahim akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa 30 wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga SHIRECU (1984) Ltd amesisitiza umuhimu wa vyama vya ushirika kuendeshwa kwa mifumo ya kisasa ya kidijitali na kibiashara.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 30 wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU 1984 LTD ), uliofanyika leo katika ukumbi wa SHIRECU,  Ibrahim ameweka wazi kwamba Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) inasisitiza vyama vya ushirika kuwa na akaunti za benki katika benki ya Maendeleo ya ushirika, na kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kidijitali kwa ajili ya kuboresha utendaji wa vyama hivyo.
Amesema mwelekeo wa uendeshaji wa vyama vya ushirika nchini lazima ubadilike ili kutoa nafasi kwa vyama hivyo kujiendesha kibiashara, kuongeza tija, na kuchangia zaidi katika uchumi wa taifa.
“Tunataka kuona vyama vya ushirika vikijiendesha kibiashara, na sio tena kutegemea tu huduma za msingi. Vyama vya ushirika lazima viwe na nguvu na viwe na uwezo wa kufanya biashara ili kusaidia wanachama wao. Mapato yote yanayotokana na vyama vya ushirika ni mali ya umma , wanachama,” amesema Ibrahim.
Ibrahim amesema vyama vya ushirika lazima viongeze nguvu katika kuzalisha mazao na kuwekeza katika miradi ya kiuchumi ili kuwa na michango inayokubalika.
Amehimiza kwamba wanachama wa vyama vya ushirika wasikubali kukaa na kulalamika, badala yake watumie rasilimali walizonazo kuboresha hali zao za kiuchumi.
“SHIRECU imekua kwa muda mrefu, lakini lazima tuondoke kwenye mazoea ya zamani ya kutoshughulika na mazao ya kilimo. Hatupaswi kukaa na kulalamika, tunazo rasilimali na nguvu za kufanya biashara kwa mafanikio,” amesema Mrajis Msaidizi huyo.
Akizungumzia ushirikiano na wadau, Ibrahim amesema  vyama vya ushirika lazima vishirikiane na wadau wa kibiashara.